CHAKULA CHA MGONJWA MWENYE KISUKARI AINA YA PILI
Chakula bora kabisa kwa mgonjwa wa kisukari ni kile ambacho ni chakula cha asili na si kile ambacho kimetengenezwa kiwandani.
Unahitaji chakula ambacho hakijakobolewa, unahitaji zaidi matunda na mboga za majani.
Kutumia vyakula hivi naenda kukueleza kwenye hii makala kutakusaidia kupata mahitaji ya viinilishe unavyohitaji wakati huo huo ukipunguza matatizo yanayoweza kuletwa na kisukari ikiwemo hatari ya kupatwa na magonjwa ya moyo.
Ndiyo, si vyakula hivi tu kwenye hii orodha ndivyo unavyopaswa kuwa unakula, bali kuvijumuisha vyakula hivi kwenye mlo wako kila siku kutakusaidia kuimarika kwa afya yako kwa ujumla.
Kama tayari unafuata mlo wenye afya wenye matunda, mboga za majani na kula vyakula ambavyo havijakobolewa naomba nikupe hongera mapema. Upo njiani kuelekea kwenye maisha ya afya bora na marefu na unaelekea kwenye hatua za kudhibiti uzito wako na kiasi cha sukari kwenye damu yako.
Vyakula hivi naenda kuvijadili siyo tu vina nyuzinyuzi za kutosha, madini, vitamini na viuavijasumu tu, lakini pia vyakula hivi vinapatikana kirahisi kwenye mazingira yetu na vinapatikana kwa bei rahisi.
Kula ugali wa dona na uachane na ugali wa sembe, kama ni mkate tumia mkate wa ngano ambayo haijakobolewa (brown bread), kunywa maji mengi bila kusahau kujishughulisha na mazoezi ya viungo kila siku.
Kisukari ni ugonjwa wa tabia, ni matokeo ya kile unachokula na kunywa kila siku.
Wapo watu hawaamini kama unaweza kupona Kisukari lakini kama utaamua kula chakula sahihi kwa muda mrefu, ukawa bize na mazoezi kila siku, ukinywa maji ya kutosha kila siku na kutumia chumvi ya kutosha kwenye vyakula vyako kila siku kupona inakuwa ni jambo la kawaida.
Kuna kila aina ya upotoshwaji na maelezo yasiyo sahihi kuhusu ugonjwa wa kisukari, hata hivyo ni ugonjwa wa kawaida ambao hautakiwi kuwa kitendawili kwako kama utakuwa tayari kujifunza ukweli na mambo mapya kupata uelewa mpya na wa kweli.
Kisukari si ugonjwa wa kuendelea kuteseka nao miaka na miaka wala hivi vyakula sijaviandika ili ndiyo iwe lishe yako kwa miaka yote, la hasha hii ni kwa muda mfupi tu wakati ukiwa na kisukari na huku ukipambana kuhakikisha unapona na kutokuwa mtumwa wa kuchagua kula hiki au hiki.
Kisukari aina ya pili ni wakati ambapo insulini inakuwa huru (insulin-indepe
ndent) au inapatikana lakini kongosho haliitoi na hivyo dawa (kemikali) lazima itumike kulilazimisha kongosho kutoa insulini.
Aina ya pili ya kisukari huanza kujitokeza kuanzia umri wa miaka 40 na kinachosababisha ni miaka mingi ya kula chakula kisicho sahihi, kutofanya mazoezi au sababu za kurithi (genetics).
Kwa bahati mbaya, nyakati hizi tunashuhudia hata watoto wadogo wakipatwa na aina hii ya kisukari. Watu wenye kisukari cha aina hii ya pili pia huwa na uzito uliozidi (overweight).
Chakula cha mgonjwa wa kisukari aina ya pili
1. Tufaa (Apple)
Kuna msemo wa kizungu unasema: ‘An apple a day keeps the doctor away’, inamaanisha kula tunda moja la tufaa kwa siku kunaondoa uhitaji wa daktari hasa daktari wa matatizo ya moyo.
Kula tufaa moja tu kwa siku kwa wiki 4 kunaweza kupunguza kolesto mbaya mpaka asilimia 40. Kuna aina ya viondoa sumu vilivyomo kwenye tufaa ambavyo huwezi kuvipata sehemu nyingine yoyote na ndiyo vinalifanya tunda hili kuwa tunda mhimu zaidi kutumika na mtu mwenye kisukari kila siku.
Tunda hili tamu limeonekana kutoa ulinzi mkubwa kwa watu wenye kisukari hasa kisukari aina ya pili. Tufaa moja dogo la kawaida lina gramu 3 za nyuzinyuzi (fiber), nyuzinyuzi ni kitu kingine mhimu kwa mgonjwa wa kisukari.
Kumbuka pia lakini tufaa moja lina wanga gramu 15 hivyo usile zaidi ya moja kwa siku.
2. Parachichi
Parachichi linajulikana kwa kuwa na mafuta mazuri kwa ajili ya moyo (monounsaturated fat).
Mafuta ya namna hii kama yanayopatikana kwenye tunda la parachichi yanaweza kuweka sawa usawa wa kolesto mwilini, yanaweza kupunguza hatari ya kupatwa na magonjwa ya moyo na hivyo kuwa tunda zuri kwa mtu mwenye kisukari.
Parachichi ni tunda zuri sana kwa mtu anayesumbuliwa na kisukari aina ya pili.
Parachichi ni tunda ambalo sababu ya mafuta yake mazuri, sababu parachihchi moja laweza kuwa na mpaka gramu 16 za mafuta linatakiwa lichukuliwe kama mafuta.
Wakati huo huo parachichi moja lina nyuzinyuzi gramu 2 na wanga gramu 2.
Unaweza kula parachichi lenyewe kama lilivyo, unaweza kuongeza kwenye kachumbali mbalimbali au ukanywa juisi yake kila siku.
3. Maharage
Maharage ni moja ya matunda au mboga za ajabu sana watu wengi hawajuwi.
Kile nataka nikujulishe kupitia makala hii ni kuwa maharage yana nyuzinyuzi (faiba) ya kutosha kwa mahitaji yako ya kila siku na si hivyo tu maharage yana protini bora kabisa kuliko zote isiyo na madhara kama ile ya kwenye wanyama na hizi ndizo sababu maharage ni chakula kizuri sana kwa mtu mwenye kisukari na mwenye shinikizo la juu la damu pia.
Vile vile kutumia vyakula vyenye nyuzinyuzi zaidi kunakuondolea hatari ya kupatwa na mishtuko ya moyo (stroke).
Inasisitizwa upate walau gramu 25 za faiba kila siku. Kikombe kimoja cha maharage yaliyopikwa kina mpaka gramu 9 za faiba.
Inashauriwa kwa watu wenye kisukari kula gramu 25 mpaka 30 za maharage machanga ya kijani kibichi au njegere (green beans), siagi halisi na chumvi dakika 15 kabla ya kwenda kulala, hii itasaidia kushusha damu sukari waamkapo asubuhi.
Maharage haya yana kiasi kidogo cha wanga (carbs), na kiasi kingi cha protini, magnesiamu na asidi amino iitwayo ‘tryptophan’ ili kuubeba mwili usiku mzima.
Jaribu kutumia maharage kama chanzo kikuu cha protini kila siku na vizuri zaidi ni kuwa yanapatikana kwa bei rahisi zaidi ukilinganisha na nyama au samaki.
4. Karoti
Zilizopikwa au zikiwa freshi ni mboga nzuri kuongezwa kwenye chakula chochote. Karoti zina kiasi kingi cha vitamini A, viuavijasumu mhimu zaidi ‘beta-carotene’.
Vitamini A ni mhimu sana kwa matatizo ya macho, kuzuia kansa na kinga ya mwili vitu viwili mhimu sana kwa mtu anayesumbuliwa na Kisukari.
Kwa mjibu wa tafiti mbalimbali hii beta-carotene inao uwezo wa kuzuia usipatwe pia na kisukari hasa kisukari aina ya pili.
Pendelea kutafuna karoti mbichi zaidi na siyo zilizopikwa kwa matokeo mazuri.
5. Samaki
Samaki ni chakula bora kwa mgonjwa wa kisukari. Samaki wana omega 3 ambayo ni nzuri kwa mtu anayetaka kuepuka kolesto na kisukari kwa ujumla.
Omega 3 pia ni nzuri kwa mtu mwenye presha ya kupanda na hupunguza uwezekano wa kutokea tatizo la kupoteza kumbukumbu na ukichaa.
Pamoja na hayo nakushauri utumie samaki wa hapa hapa kwetu Tanzania na siyo wale kutoka nje kwani wengine wanavuliwa kwa namna ambayo si salama kwa afya.
Kula samaki kila mara kama unasumbuliwa na kisukari.
6. Kitunguu swaumu
Kitunguu swaumu ni kiungo kizuri kwa chakula sababu ya harufu yake nzuri ya kupendeza na wakati huo huo ni dawa nzuri sana kwa magonjwa mbalimbali mwilini ikiwemo kisukari.
Kitunguu swaumu kwa miaka mingi kimetumika kutibu kolesto, magonjwa ya moyo, shinikizo la juu la damu na kansa. Hizi ndizo sababu zinazokifanya kitunguu swaumu kuwa chakula bora kwa mtu mwenye kisukari
Hata hivyo ili kitunguu swaumu kiwe kizuri kama tiba ni vizuri kitumike kibichi yaani bila kupikwa katika moto.
Katakata punje 3 za kitunguu swaumu na unywe na maji vikombe viwili kama unavyokunywa dawa nyingine za kawaida kila unapoenda kulala.
Ukishakuwa umevikatakata inashauriwa uviache kwanza katika hewa kwa dakika 10 ndipo umeze kwa matokeo mazuri zaidi.
7. Tikiti maji
Ukipata hamu ya kutaka kula au kunywa chochote kitamu hasa hivi vya dukani basi wewe kimbilia kula tikiti maji au hata juisi yake.
Kama ilivyo kwa nyanya, tikiti maji pia lina viuavijasumu mhimu sana (lycopene) ambavyo vinaweza kusaidia kukukinga dhidi ya baadhi ya kansa na kudhurika kwa seli kunakohusiana na magonjwa ya moyo.
Tikiti maji pia ni zuri pia kwa mtu mwenye kolesto.
8. Mbegu mbegu
Mbegu mbegu ndivyo vyakula bora zaidi kwa mtu mwenye Kisukari. Mbegu nyingi zina mafuta ya omega 3, nyuzinyuzi (faiba), vitamin E. Vitu Hivi ni mhimu kwa mtu mwenye kisukari hasa kisukari aina ya pili.
Sababu mbegu mbegu hizi hazihitaji friji ni rahisi kubebeka popote unapokuwa.
Pamoja na hayo nakukumbusha kula kwa kupima kabla hujala ili usije ukala nyingi kupita kiasi kama utakuwa unachota moja kwa moja toka katika kikapu.
Mbegu mbegu ninazoziongelea hapa ni pamoja na mbegu za maboga, korosho, karanga, lozi, alizeti nk
Ujazo wa kikombe kimoja cha kahawa kwa siku kwa mbegu hizi unatosha.
Epuka mbegu hizi zikiwa na chumvi sana, au zikiwa na sukari sana au zimeongezwa chokoleti sababu vitu hivyo vinaongeza wanga, nishati na chumvi vitu ambavyo si vizuri sana kwa mgonjwa wa kisukari.
9. Vitunguu maji vyekundu
Vitunguu maji ni chanzo kizuri cha viuavijasumu (antioxidants), nyuzinyuzi, na folate vitu vizuri sana kwa afya ya moyo.
Vitunguu maji vina kiondoa sumu mhimu sana kiitwacho ‘flavonoid’ ambacho ndicho hupigana dhidi ya kansa na magonjwa mengine kwenye mfumo wa upumuwaji kama vile pumu.
Ukiweza kula vitunguu maji katika kachumbali kila mara na usivioshe na chumvi, ule ukali wake ndiyo dawa yake yenyewe.
Na vitunguu maji ninavyoongelea hapa zaidi ni vile vyekundu.
10. Pilipili hoho nyekundu
Pilipili hoho nyekundu ni pilipili hoho za kawaida ila tu zinakuwa zimeachwa shambani zikomae kwa muda mrefu zaidi. Pilipili hoho nyekundu zina viiinilishe mhimu ikiwemo kiuakijasumu vitamin C, lycopene na beta-carotene.
Pia zina vitamini A na C ambazo kwa pamoja zinahamasisha afya bora na kupunguza hatari ya kupata magonjwa ya moyo, kisukari na baadhi ya saratani.
Unaweza kuwa upo bize na vidonge vya multivitamins lakini tafiti zinaonyesha vidonge hivyo haviwezi kufanya vizuri kama vile ukila vyakula kamili kama hivi ninavyoelezea kwenye hii makala.
11. Spinachi
Spinachi ni chakula kizuri kwako. Pengine tayari unafahamu kwamba spinachi ina vitamini nyingi na madini mbalimbali.
Spinachi ina vitamini C, A, folate na beta-carotene. Bakuli moja ya spinachi kwa siku inakutosha. Spinachi ni nzuri pia kwa kuzilinda seli dhidi ya vijidudu nyemelezi ambavyo vinapelekea magonjwa sugu na kuzeeka mapema.
Watu wanaokula mboga za majani zenye rangi ya kijani wanapata kinga dhidi ya kisukari kwa zaidi ya asilimia 14 hasa wenye kisukari aina ya pili.
Spinachi inapatikana kirahisi karibu kila sehemu hapa Tanzania na kwa bei nafuu kabisa.
12. Nyanya
Nyanya ni chanzo kizuri cha vitamini C na A, pia zina kiondoa sumu mhimu sana kiitwacho ‘lycopene’. Nyanya ni chakula kizuri dhidi ya kansa mbalimbali hasa tezi dume.
Habari njema ni kuwa kiondoa sumu ‘lycopene’ kinahusika moja kwa moja na udhibiti wa ugonjwa wa moyo.
Nyanya zimethibitika kuwa dawa nzuri dhidi ya maambukizi sababu ya kuwa na viinilishe mhimu viwili vijulikanavyo kama ‘carotenoids’ na ‘bioflavonoids’ ambavyo vinahusika pia na kupunguza hatari ya kupatwa na magonjwa ya moyo ugonjwa ambao unatesa watu miaka ya sasa.
Kwenye hili, nyanya nzuri ni ile iliyopikwa ndiyo inayo hii ‘lycopene’ kwa wingi kuliko nyanya freshi.
Bado nakushauri usitumie nyanya za kwenye makopo au za dukani zilizotengenezwa viwandani.
13. Mtindi
Mtindi ni chakula kingine kizuri kwa ajili yako. Ni chanzo kizuri cha kalsiamu ambayo husaidia kuimarisha afya ya mifupa yako na meno pia kujenga na kuimarisha kazi za misuli na mishipa ya damu.
Ni chanzo kizuri pia cha vitamini B2 (riboflavin) na protini.
Mtindi huwa na bakteria wazuri kwa afya yako hasa kwa ajili ya kuongeza nguvu katika mfumo wa mmeng’enyo wa chakula na kuimarisha kinga ya mwili.
Mtindi ni mzuri kwa mtu anayetaka kujikinga hata kujitibu na kisukari aina ya pili.
Mtindi hushusha kolesto na kutengeneza vitamini maalumu ambazo husaidia kudhibiti kisukari. Vitamini D, madini ya kalsiamu na magnesiamu katika mtindi ndivyo vitu vinavyoufanya mtindi kuwa chakula kizuri kwa mtu mwenye kisukari aina ya pili.
Mhimu, pamoja na kuwa mtindi ni chakula kizuri kwako bado unatakiwa usitumie zaidi ya kikombe kimoja kwa siku (robo lita), pia ni mhimu upate mtindi uliouandaa nyumbani kuliko wa dukani na wakati huo huo kama utanunua dukani hakikisha usiwe umeongezwa kitu kingine chochote ndani yake na uwe na mafuta machache au usio na mafuta kabisa.
0 Comments