Header Ads Widget

KAMA WEWE U MIONGONI MWA WATU WA KIZAZI LAINI-LAINI BASI SAHAU KUHUSU MAFANIKIO

KAMA WEWE U MIONGONI MWA WATU WA KIZAZI LAINI-LAINI BASI SAHAU KUHUSU MAFANIKIO
Toka kuumbwa kwa dunia kumekuweko watu waliofanikiwa na watu wasiofanikiwa. Kumekuweko kizazi cha watu wachache jasiri na wenye uthubutu wa kweli na kizazi cha watu wengi laini-laini ambao kwao mambo yanapaswa yatokee tu kama wanavyotaka bila wao kuyaleta.
Kumekuwako kizazi cha watu wachache waliotaka kujua ukweli hasa wa mambo upoje licha ya "uhalisia" unaohubiriwa, na kumekuweko kizazi cha watu wanaosema "hali iko hivi" (yani uhalisia uko hivi) na hauwezi kubadilika mpaka mtu au watu fulani waibadili.
Kumekuwako watu wanaosema "Wazazi wangu wange....basi ningefanikiwa. Au Serikali iki...... nitafanikiwa. Bosi wangu akiniongeza mshahara....nitafanikiwa. Nikipata mkopo nitafanikiwa kufanya hivi na vile. Nikilipwa na wateja wangu mapema nitafanikisha hili.
Au anasema: Mimi ningeshaanzisha saluni yangu lakini... Ama: Aisee ninataka kuwa mwanamuziki mkubwa lakini....
Umeona? Kizazi chenye "kama ingekuwa hivi". Kizazi chenye litania ya sababu kwa nini mafanikio ni magumu kwao. Hiki ndiyo kizazi laini ninachokiongelea.
Kama umebahatika kusikia ndoto za watu wengi hapa duniani unaweza kushangaa jinsi watu walivyo na ndoto kubwa ambazo zinaweza kumaliza matatizo mengi tuliyonayo.
Na yumkini wewe pia una "mandoto" ya kufa mtu. Yani ukiangalia ndoto zako daah unajisemea aisee "ipo siku ntakuwa balaa". lakini jiulize swali moja tu:
JE WEWE NI MMOJA WA WATU LAINI?
Kama jibu ni NDIYO basi sahau kufanikiwa!
Mafanikio hayapo kwa ajili ya watu laini.
Unanisikia?
Mafanikio hayakuumbiwa watu watu laini. Mafanikio siyo kitu kinachokuja kama upepo tu kutoka kusikojulikana. Mafanikio ni kitu unachopaswa #kukitafuta na kukiendea na mpaka ukipate unatakiwa uwe mgumu kwanza.
Usifikiri ni swala la kuomba Mungu tu. Unaweza kupiga magoti ukiomba Mungu ufanikiwe lakini kama wewe upo katika kundi la watu laini basi utaota sugu za magoti bure.
Nimewasoma watu waliofanikiwa na bado naendelea kuwasoma wengi zaidi na naweza kukwambia wote niliowasoma hadi sasa ni watu WAGUMU. Imara. Wasiolialia wala kulalamikia hali ya maisha wala kuongelea "uhalisia".
Watu kama Jack Ma, watu kama Nelson Mandela, watu kama Mohamed Dewji, Donald Trump, watu kama Jim Rohn watu kama Margareth Thatcher watu kama Abraham Lincoln watu kama Aliko Dangote. Hawa ni watu WAGUMU!
Angalia toka enzi na enzi, hivi baba yetu wa imani mzee Abraham alikuwa MTU LAINI?
Vipi kuhusu Musa?
Mtu anaweza kufunga siku 40 usiku na mchana na akarudia tena hilo zoezi mara ya pili akiwa ni mtu laini laini?
Wewe ukifunga siku mbili unaanza kusikilizia tumbo na kichwa. Kwa sababu wewe ni mtu laini.
Hivi Christopher Columbus alikuwa laini laini? Mtu unaweza kupotea baharini halafu unaosafiri nao wanakutishia kukuua kila wakati na unajua wako makini na hilo... na bado unaendelea kuwaongoza vizuri mpaka mnafika na wanafurahi kuliko hata wewe?
Hivi kweli mwalimu Nyerere alikuwa laini laini?
WATU WAGUMU.
Watu wanaofanikiwa huwa hawana kawaida ya kuishi kwenye eti uhalisia.
Na ngoja nikuambie kitu rafiki. "Uhalisia" ni kitu BINAFSI. Unaweza kuwa katika watu wanaosema maisha ni magumu lakini kwako uhalisia ukawa tofauti.
Mimi ninajua watu ambao walikuwa na hali ngumu kiuchumi na wamefanikiwa kirahisi wakati huu wa JPM ambao watu wanaimba eti hali ngumu. Endelea kuimba ukimaliza beti zote urudie tena wimbo wa hali ngumu uone kama maisha yako yatakuwa yamebadilika kwa kuimba hali ngumu.
Uhalisia ni kitu binafsi.
Unaweza kuwa kati ya watu wenye furaha na amani na ukawa na wasiwasi na kesho. Na unaweza kuwa kati ya watu wasio na furaha na wanaolalamika na ukawa mtu mwenye mawazo chanya na furaha.
Lakini utatakiwa kuwa mtu mgumu kwanza. Lazima uachane na tabia za kitoto za kulialia.
Usifikiri Mungu anabadilisha formula zake kwa sababu ya kulalamika kwako wiki nzima halafu wikendi unaenda kumwimbia nyimbo za taratibu kanisani.
Ukweli ni kuwa ukizidi kulalamika Mungu anafika mahali anachukia na anaweza kukufuta kabisa. Maana akili yako inakuwa imeanza kupoteza uwezo iliyoumbiwa wa kuwa na ubunifu na mawazo chanya. Kazi ya changamoto maishani mwako ni kuamsha ubunifu ndani yako. Sasa ukilalalamika tu Mungu anakuona wewe ni mjinga kabisa!
Kumbuka kuna KIZAZI cha taifa fulani Mungu aliwahi kuzuia kisifikie walikokuwa wakienda kabisa sababu ya kulalamika. Mungu kawatoa utumwani wanalalamika. Kawavusha bahari ile kuwajaribu kidogo tu wanalalamika. Kawajaribu tena kuona kama wanamwamini zaidi wanazidi kulalamika tu.
Akakaa kimya na kiongozi wao mwezi mmoja na siku 10 tu wakaanza mchakato wa kupata "mungu" mpya! Khaa. Kwa kuwa Mungu HANAGA kawaida ya kushindana na wanadamu akazuia tu hawa hawaingii kamwe Kanaan aisee ni bora waingie watoto wao kuliko hawa.
Kulalamika.
Hayo ndiyo matokeo ya kulalamika na kukasirikakasirika tu usipopata unachotaka - yaani unakuwa huna tofauti na mtoto!
Yaani usipopata unachotaka badala ya kuwa mbunifu unatafuta wa kumlaumu huku umekasirika. Mungu atakuchukia sana yani.
Tuna wimbi kubwa la watu walaini laini siku za leo. # Whiners and #crybabies! Watu wanaolialia tu. Ooh nimeomba nauli sijapewa sasa mi ntaendaje! Tafuta njia nyingine wewe.
Oh nilitaka kuja ila mvua ikanyesha sasa ningefanyaje? Khaaa!
Wewe ni mtu laini rafiki yangu!
Oh "Nimeomba kazi sijaitwa yaani serikali hii imezuia ajira sijui tutaishije nchi hii mi nachukia sana".
Unaonyesha jinsi ulivyo mtoto! Mtaishije wewe na nani kwanza?
Ooh, "Tumemaliza JKT hakuna ajira mtupe ajira tusije kuwa majambazi kwa nini hamtupi ajira".
Utoto tu! Huko JKT mlienda kujifunza kuandika CV za kazi kwani? Kawe jambazi tu wakumiminie risasi hadi ufe maana sasa hivi hawana muda wa kukamatanakamatana ni VITA, utakamatwa tu endapo ukijisalimisha.
"Ooh ninataka kujiajiri lakini sina mtaji serikali yenyewe haijaleta viwanda walitudanganya tu!"
Tafuta njia nyingine wewe!
Oh "mi natamani kuwa mbunge lakini huko mpaka umjue MTU"
Upo makini kweli wewe? Ni kwamba tu hujuwi ni nini hasa unachokihitaji rafiki.
Kizazi laini!
Oh "mi ninataka sana kusaidia yatima lakini sina uwezo!"
Usitudanganye unataka kusaidia yatima wewe.
Kwanini usiende kuwasaidia kupiga deki?
Nani alikuambia kuwa msaada ni hela tu?
Kwanini usijitolee kwenda kuwafundisha twisheni au kuwafundisha muziki au kucheza nao tu, kwani huo si ni msaada wa kisaikolojia mzuri zaidi kuliko kwenda kuwapelekea biskuti na peremende na kupiga nao picha ili ukapost Instagram!?
Kawaombe kupiga deki wikendi uone kama watakataa. Hapo unaanza kujihurumia na kuhesabu gharama. Sababu wewe ni mtu laini.
Yani kila kitu ooh mimi, oh unajua, yani hii hali, yani uchumi, kama ningekuwa na wazazi, oh kama ningesoma..
Kizazi laini!
Wengine huwa wananambia unajua kaka wewe hujui tu maisha yangu. Na mimi huwa nawaambia WALA SIHITAJI KUJUA maana haturudi nyumawe na hata wewe hujui ya kwangu. Si ni kweli?
Ninachojaribu kukuambia hapa ni kuwa usipoacha kuwa laini na mtu wa kulalamika lalamika basi utafika mwisho wa maisha yako unalalamika tu na kukasirika huna kitu cha maana umefanya duniani hapa.
Ukiambiwa jisomee vitabu ooh unajua mimi, muda, nachoka sana, narudi usiku sana.
Kizazi laini!
Unajihurumia.
Hutaki kujitoa mhanga.
Mkufunzi wangu aliniambia mwaka juzi kuwa kama huwezi kujitoa mhanga kwa
# USINGIZI au #CHAKULA hivyo vitu viwili basi mafanikio kwako ni ndoto hata mafanikio ya kiroho.
Mtu makini sana huyo, nampenda sana huyu mkufunzi wangu
Na ndiyo maana kuna vitabu lukuki vimeandikwa kukwambia cha kufanya ili ufanikiwe katika nyakati zinazoitwa ngumu.
Lakini wewe unaweza kukesha kusubiri matokeo ya mpira au kuangalia mfulululizo wa tamthiria kuliko kusoma kitabu cha namna gani ufanikiwe kutimiza ndoto zako. Eti ooh siyo vitu ambavyo mimi navipenda. Kwa hiyo kukesha unakodolea macho TV ndiyo vitu unavyovipenda maishani? Kupenda? Na mafanikio yatakujibu hivyohivyo wewe siyo watu ninaowapenda, wapo wenyewe kwa ajili ya mafanikio siyo wewe!
Hivi unawezaje kukaa saa tano ukisubiri uangalie mpira ligi ya Ulaya halafu ukashindwa kukaa hadi saa tano ukiandaa mipango yako.... halafu unataka ufanikiwe?
Mungu siyo mjinga rafiki. Biblia inasema Mungu hadhihakiwi. APANDACHO MTU NDICHO ATAKACHOVUNA.
Hivyo kama umeshapanda ujinga na kulalamika aisee ving'oe haraka sana!
Leo hii magroup mengi ya WhatsApp hayakujengi lakini unapenda kukaa humo. Vitu unavyosoma na kuweka akilini mwako kutoka kwenye hayo magroup vinaua safari yako ya mafanikio lakini hutaki kuviacha. Ajabu ukiambiwa kuna group la kusaka mafanikio unasema "na mimi jamani niungeni".
Sababu ni kweli unatamani kufanikiwa. Lakini ukiwekwa kwenye hilo group halafu ukaambiwa jamani eeh humu kwenye group kila siku jioni lazima kila mtu aseme amejifunza nini kwenye kitabu anachosoma kwa sasa, heee group linageuka kuwa chungu.
Halafu unataka mafanikio!
Hapana rafiki, mafanikio hayatakuja kwako kamwe!
Sababu wewe ni mtu laini sana.
Ukiambiwa kuna semina ya bure kujifunza ujasiriamali unasema ooh muda sina, ooh mbona mmeweka muda mbaya muda huo ndiyo nakuwa natoka kazini. Lakini ukiambiwa kuna Fiesta usiku wa manane na kuna kiingilio elfu 20 siku hiyo hata kazini unatoroka mapema ili uwahi kukaa (I MEAN KUSIMAMA) mbele karibu na jukwaa na kupigwa na umande mpaka asubuhi huku ukichekacheka watu wanaokata viuno!!
Bakhresa alianza hivyo?
Dewji alianza hivyo?
Mengi alianza hivyo?
Nani unayemjua amefanikiwa na alianza safari yake ya mafanikio hivyo?
Halafu baadaye unashangaa hela huna unakimbilia kucheza BIKO na TATU MZUKA na kubet matokeo ya Manchester na Arsenal sijui Barcelona.
Huo muda ungekuwa umekaa unajifunza mambo muhimu ungefika mbali sana! Wengine nyie ni mabilionea wakubwa wa baadaye lakini NI WALAINI MNO! Mpaka hapa mtu anasoma halafu anasema duh ndefu! Unataka vitu vya kudumaza AKILI yako tu.
Mungu amenipa karama ya kuandika nikuandikie vitu vya msingi nalala kwa kuchelewa naamka alfajiri ili nikuandalie kitu cha kukusaidia BURE lakini uwezo wako wa kufikiri unakutuma kusema hii makala ni "NDEFU". Hujui kuna watu wanatamani wapate tu makala hii moja tu na maisha yao yatabadilika KABISA lakini hawaipati.
Basi sawa wewe kasome fupi fupi ziko nyingi tu mbona.
Lakini nakuambia hutafanikiwa kwa kusoma dondoo fupi fupi. Bill Gates hawezi kusoma vitabu 50 kwa mwaka halafu wewe ukasome dondoo za Instagram na vipichapicha vyenye NUKUU ZA MAFANIKIO halafu mfanane mafanikio!
Mungu atakupaje mafanikio?
HAUPO TAYARI!
NI MLAINI SANA!
Watu niliokutajia pale juu ni WATU WAGUMU.
ACHA KUWA MLAINI RAFIKI.
Kama unataka kufanikiwa lazima uwe MGUMU kwanza kabla hujaanza safari ya mafanikio.
KWANINI?
Sababu utakumbana na changamoto njiani, utakutana na watu wa kukukatisha tamaa wengi mno. Utafika mahali inahitaji uendelee mbele lakini kwa sababu wewe ni mlaini utaachia njiani.. Mtu anaanza biashara yake kisha miezi mitatu tu anaacha!
Sababu ni walaini sana.
Mafanikio hayapo kwa ajili ya watu laini na wenye kulia lia!
Unalialia tu.
Utafika uzeeni una Ph.D ya kulialia! Utapoteza nafasi ya kuwasaidia wengine kufanikiwa kwa sababu ulichagua kuwa MLALAMISHI na MTOTO.
Ukasahau UNATAKIWA KUWA MGUMU ILI KUPATA VITU UNAVYOHITAJI MAISHANI. Unaishi kwa "MAWAZO YA WATU".
Kwa kuwa wengine wanalalamika basi unadhani na wewe uliumbwa kulalamika kama wao! Unaanza kuwa mbobezi wa kujihurumia na kuomba huruma za wengine. Ndo maana unashangaa mtu anakuja Facebook kila siku status zake mara:
"Homa hii itaniua jamani". Si ikuue tu uone kama watu hawataishi. Homa yako inamhusu nani humu facebook. Huna ndugu uwaambie kuwa homa inakuua?
Mvua ikinyesha tu ooh "jamani hii mvua si ikanyeshe Mtera?" Khaa! Mungu anakuangaliaaa..anakuacha tu. Kwa hiyo Mungu hajui kama kuna mtera?
Jua likiwaka sawasawa unaona status eti "Arrrgh hili joto litatuua". Khaa. Si utembee na maamvuli ujifunike? Eti "Eh si watu watanishangaa".
Khaaa!
Haya mara mwingine kaandika: Jamani "Baba Jesca" punguza kidogo hali imekuwa ngumu mno!
Ndo hapo unashangaa mzee ndo anaongeza kaspidi gavana kidogo anabinya kidogo zaidi anakaza zaidi. Hahaaaaaa. Hapo ndo utajua kama ile mikia ya pweza hivi ni mikia au miguu, au mikono?
Sasa wewe endelea kusubiri raisi mwingine. 2020 au 2025. Si mwakani tu uchaguzi. Utashangaa mambo yanakuwa hivi hivi. Hapo unashangaa na kujiuliza hawa wenzangu waliofanikiwa wamefanyaje?
Wamefanyaje?
Nitakueleza wamefanyaje:
Walichagua kutokulalamika na kuwa wabunifu...
Walichagua kutotegemea serikali na kujitegemea wenyewe...
Walichagua kujifunza mapema...
Walichagua semina za mafanikio badala ya fiesta...
Walichagua kuahirisha "starehe" kwanza...
Walichagua kutoa muda wao wa kustarehe na kupumzika wakaamua kupigana kufa na kupona bila kujali lolote wakati wewe ulipokuwa unatukana serikali kwenye mitandao...
Walichagua kujitafutia njia za kutengeneza kipato wakiwa chuo wakati wewe ukichagua kutegemea siasa na kusubiri mkopo na ajira...
Walichagua kuonekana wajinga wakati wewe ukila bata...
Walichagua kuomba Mungu kila wakati mpaka usiku wa manane wakati wewe ukisubiri kuombewa na kuonewa huruma na kuwekewa mikono na nabii naniliu...
Walichagua kuanza kidogo chini wakati wewe ukisubiri ukafanye digrii ya pili kwanza...
Walichagua kuamini katika kujibidiisha na kujituma ili kubadilisha maisha yao na vizazi vyao wakati wewe ukiridhika na ulipo sasa...
Hapo ndo utajua kama utakula mijadala uliyokuwa unapoteza nayo muda sijui Wema Sepetu sijui Boss Lady. Hapo ndo unabaki unakasirikia waliokupita kimafanikio. Unawachukia bila sababu.
Unabaki kushabikia siasa na Simba na Yanga. Hapo muda umeisha utu uzima umekukuta.
Hapo ndo utajua Fiesta ina uwezo wa kukufanikisha au la. Ndiyo hapo jibu utakuwa nalo!
Kwahiyo achanana na mawazo ya watu wanaolalamika.
Itakupoteza.
FIKIRI KWA AJILI YA USTAWI WAKO.
Na hata hivyo kama kweli hali imekuwa ngumu kwako kama usemavyo basi nikushauri tafuta kakitabu kinaitwa TOUGH TIMES NEVER LAST BUT TOUGH PEOPLE DO.
Utaelewa nachosema. UNATAKIWA KUWA MGUMU KULIKO HALI YAKO ILIVYO SASA.
Muda unaotumia Facebook, Instagram na Snapchat au WhatsApp ungeutumia vizuri mbona ungesaidia watu wengi mno! Hivi unadhani Mungu atakusahau kweli wakati anaona unatumia muda wako vizuri kujifunza mambo muhimu?
Lakini vijana wengi ninawaona humu kwenye mitandao wakikuta mada kama hizi wengine wanatukana wengine WANAJIDAI KUJUWA SANA, wengine WANADHARAU tu wanataka kila post iwe inaongelea vitu LAINI LAINI tu. Tunazalisha taifa la walalamishi na MITOTO! Watoto wadogo wanajifunza kwa kuona.
Wasomi wengi vyuo vikuu ni walalamishi na WATOTO. AIBU! Ndo maana unashangaa mtu anamaliza chuo akitaka kwenda kusambaza CV anaomba nauli kwa wazazi. Yani kama elimu ya Chuo Kikuu inashindwa kukuzalishia nauli wewe itamsaidia nani sasa? Utasikia eti. Ah sasa bro sijapata kazi si unajua tena. Ulalamishi tu. Si ukafundishe hata twisheni? Ni aibu! Wasomi ndiyo wanaenda kuwa watendaji. Wabunge. Unashangaa analalamika tu.
KWANINI? > KIZAZI LAINI.
Nakuambia rafiki utakuwa mbunge au waziri na utaondoka hukumbukwi. Sababu hukugusa maisha ya watu. Haukufanikiwa. Sababu ulikuwa mlalamishi na mtoto maisha yote.
Ndiyo unashangaa mtu mzima anaachishwa kazi anaanza kulia hadharani. Eti ntaishije? Ni aibu.
Na hivi ndivyo jamii yetu inavyoanza kujizoesha na kuwa kadri siku zinavyoenda!
You need to be TOUGH. UNATAKIWA KUWA MGUMU
Mgumu kwa ajili ya ndoto ulizonazo.
Mgumu kwa ajili ya wanao.
Mgumu kwa ajili ya wengine
Mgumu kwa ajili ya nchi yako
Mgumu kwa ajili ya dunia
Mgumu kwa ajili ya Mungu
Mgumu kwa ajili yako mwenyewe
Mungu hakukuumba uje ulie toka unazaliwa mpaka unakufa. Mungu alikupa uwezo wa kusimama imara katika kila hali na changamoto. Lakini umechagua kulialia. Yaani umekuwa mtu wa: Ooh yani sijui nianzie wapi?
Yani utadhani mwili wako umekufa ganzi kuanzia shingoni kwenda juu!
Acha kuwa mlaini sana rafiki.
Kama uko kwenye kundi la watu laini bonyeza kitufe cha KUTOKA haraka sana.
Toka humo.
Jifunze kuwa mgumu na upigane kwa yale unayoyataka. Siyo kulalamika.
Hakuna jambo unaweza kulibadili kwa kulalamika na kulialia.
ACHANA NA KUTUKANA SERIKALI HAIKUSAIDII.
Sisemi uisifie. Hiyo ni juu yako. Nachosema kuitukana haibadilishi kitu maishani mwako.
Mafanikio hayapo kwa ajili ya watoto na walalmishi tayari nimeshakueleza hilo.
Achana na kusoma kurasa za watu wanaolalamika na kukasirika kila siku.
Haikusaidii kusikiliza watoto wanaolia.
Amua kusema maneno haya:
"Kuanzia leo sitaki kulalamika. Wala kusikiliza malalamiko. Lakini nitapigana kwa ajili ya ndoto zangu, nitapigana kwa ajili ya mafanikio yangu, nitasonga mbele kama mwanajeshi mpaka nifanikiwe. Sababu mimi ni mwana wa Mungu na Mungu hashinwi kamwe na katika ufalme wa Mungu kamwe hatulalamiki lalamiki kijinga".
Amua kwamba kuanzia leo nikikosa kitu nachotaka sitakasirika wala kulalamika bali nitakuwa mbunifu na kuwaza upya ili nikipate hicho hicho nilichotaka. Anza kujifunza tabia ya kuwa MTU MGUMU. Kajifunze kwa machinga. Akitembeza viatu watu 10 mfululizo kawaonyesha na wote hawanunui hakati tamaa na kurudi nyumbani baada ya masaa mawili. Atakaa kitaa siku nzima akiendelea na kazi. Anajua atauza tu.
HAO NI WATU WAGUMU!
Mafanikio hayapo kwa watu laini na wanolialia.
Kuwa mgumu rafiki! Na kama wewe ni mzazi waambie watoto wako mapema. Itawasaidia kujua hilI mapema.
Kama wewe ni mlaini sahau kufanikiwa iwe ni shuleni iwe ni katika biashara, iwe ni kwenye siasa, iwe ni kwenye michezo au jambo lolote mhimu maishani – mafanikio ni kwa ajili ya watu wagumu.
Kwahiyo amua kuwa imara! Bila kujali nini kinaendelea.
Ondoa hiyo programu ya kulalamika kwenye ubongo wako. Weka programu nyingine mpya ya kuwa imara na kung'ang'ana.
BAADA YA HAPO TU NDIYO UTAWEZA KUWA MTU MWENYE MAFANIKIO!
Badilika!
Nakutakia wiki njema! Na mafanikio makubwa mwaka huu 2019 na miaka mingine ijayo.
Semper Fi,
Andrea G. Muhozya
Entrepreneur & Business Trainer
Dar es Salaam, Tanzania
East Africa.

Post a Comment

0 Comments